NI mwimbaji anayekuja juu, mwandishi wa nyimbo, mwanamitindo na baba wa
aina yake, ambaye ni mkazi wa New York na Los Angeles nchini Marekani.
Baba huyu wa mtoto mmoja, Benny Harlem, kwa kipindi kifupi ameweza
kuiteka mitandao kama vile Instagram, shukrani zikiendea aina ya nywele
zake, kujivunia rangi ya ngozi yake nyeusi sambamba na bintiye mpendwa.
Harlem na bintiye mwenye umri wa miaka sita, Jaxyn daima wameonekana
pamoja katika mitandao ya kijamii na hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa
wengi kwa namna ya mitindo yao inayoendana.
Ni hali iliyowafanya wajichotee mamia kwa maelfu ya wafuasi kutokana na
haiba yao hiyo na kuonekana kana kwamba hawatenganishwi angalau kwa
sekunde moja.
Jarida la Paper liliwahi kuzungumza naye kuhusu mvuto wao katika
intaneti, wanavyolinda mwonekano wa misuli na ukakamavu wake pamoja na
weusi wa ngozi yake katika Marekani ya leo na siri ya mafanikio ya
nywele zake.
Baba huyu anasema hupenda kuonesha mfano mkubwa kwa msichana wake mdogo katika masuala ya kujiamini na kukumbatia asili yake.
Aidha, kutokana na uzoefu wake wa malezi aliyopitia nyuma, anataka
kuelimisha jamii kwa vitendo hasa kwa wababa wenzake kuwapenda watoto
wao na kuwapa mwongozo utakaowasaidia maishani.
Benny anasema kazi yake kama mzazi ni kumlinda na kumkuza mtoto wake
huku akiwa na matumaini kuwa Jaxyn atakuwa msichana mwenye nguvu na
kujiamini.
“Binti yangu ni mzuri na ninatarajia atakuwa mwanamke mrembo, lakini
namfundisha ajipende yeye kwanza. Haelekezi macho kwa wanaume, au
kuangalia televisheni au marafiki zake.”
Dogo Jaxyn anaonekana kuwa na imani na daima mwenye furaha kwa rangi ya
ngozi yake, hivyo huwezi kukana kuwa babake anafanya vyema katika kazi
yake ya uanamitindo.
Kuhusu siri ya nywele zao, anasema wanaziosha kila wiki, wanatengeneza
shampoo na vitu kama hivyo kwa kutumia viungo vya asili kama vile mafuta
ya nazi na kadhalika na kuwa hakuna kitu kikubwa zaidi ya hilo na
matunzo mazuri.
Anasema binti yake Jaxyn anakumbana na wakati mgumu awapo shule, ambako wasichana hujaribu kuzishika nywele zake.
Kwa vile nyumba ameweka sheria ya kutoruhusu yeyote kugusa nywele zao,
bintiye huyo anaendeleza utaratibu huo awapo shuleni, kitu ambacho mara
nyingi ni changamoto mno kukizuia.
Anasema; “Watu wanatutazama na kutuuliza iwapo kweli ni nywele zetu
hasa zangu ni za asili au za kupandikiza. Jibu tunalowapa ni ndio. Kwa
kweli wengi wameondokea kuzipenda pamoja na kuwa kuna wachache walio
kinyume na hilo.
“Naona fahari ya kuwa hivi nilivyo.”
Hata hivyo, Harlem hajapitia mapenzi ya ubaba kama anayoonesha kwa
bintiye, kiasi cha kuwa mfano kwa wababa wengi wanaomfuatilia mtandaoni.
Benny (27) ambaye alianza kukuza nywele zake tangu akiwa na umri wa
miaka 15 anasema: “Binafsi sikuwahi kukutana na baba yangu hadi
nilipokuwa na umri wa miaka saba. Wakati huo baba alikuwa kocha wa mpira
wa miguu katika shule ya juu ya sekondari, hivyo mimi na familia
yangu––yaani mama, shangazi na bibi yangu tulienda uwanjani na kusubiri
hadi mpira ulipomalizika. Tuliingia kiwanjani na shangazi yangu
akamwambia baba, ‘Hey! huyu ni mwanao.”
“Baba aliniangalia kwa sekunde 10 na kisha akasema, sina mtoto hapo. Ni
kauli ninayoikumbuka sana na iliniuma sana kipindi kile” anasema
taratibu kwa vituo kila baada ya maneno machache.
Anasema ni alihisi uchungu wa kukataliwa hasa ukiongeza namna alivyokuwa
akiingiwa na wivu wa kuwaona watoto wenzake wakiwa wameshikwa mikono na
baba zao matembezini na wanapopelekwa au kurudishwa nyumbani kutoka
shuleni.
Baadaye, ili kuziba pengo hilo aliamua kuachana na hilo na kukubali hali
halisi. “Nilijitegemeza zaidi kwa wanawake, ambao wametawala katika
familia yetu. Nilikulia katika mazingira yenye wanawake watupu na mimi
nilikuwa mwanaume pekee katika familia yetu licha ya kwamba nilikuwa na
wajomba wachache mno.
“Kwa sababu hiyo niliwachukulia kina David Bowie (mwimbaji na mcheza
filamu) na Tupac Shakuru (mwanamuziki wa rap ambaye ni marehemu) kama
wababa wangu,” anasema Harlem, ambaye hakuna popote katika mitandao
anakozungumzia mkewe au rafiki yake wa kike au kwa maneno mengine mama
wa bintiye Jaxyn .
Tags
UTAMADUNI

