Jamii ya Kimaasai na ufugaji nyuki
Arusha, Tanzania
Jamii ya Kimaasai ambayo kwa
miaka mingi imekuwa ikijulikana kwa ufugaji wa mifugo mbalimbali ikiwemo
ng'ombe, mbuzi na hata kondoo hivi sasa inaonekana kubadilisha mfumo wa maisha
na kujikita katika shughuli nyengine tofauti na ufugaji.
Kuna sababu kadhaa
zinazochangia mabadiliko haya, lakini miongoni mwao ni ile inayotokana na
changamoto zilizopo katika ufugaji, hasa kiangazi kikali, uhaba wa malisho,
migogoro kati ya wafugaji na wakulima, bila kusahau athari za mabadiliko ya
tabia nchi, ikiwemo hali ya ukame, au mvua zilizopitiliza.
Mabadiliko haya yameanza
kushuhudiwa katika vijiji vya Esilalei wilayani Karatu na Monduli katika mkoa
wa Arusha, kaskazini mwa Tanzania. Baadhi ya wanawake wa jamii ya Kimaasai
wameanza shughuli za ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali kama sehemu ya
kujikimu kimaisha.
Hili ni kundi la takriban
wanawake 30 ambao hivi sasa wamekuwa sehemu ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima
Mkoani humo, maarufu MVIWARUSHA. Baada ya kuwezeshwa na Mtandao huo pamoja na
kupewa mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki, hivi sasa wanaweza kuzalisha na
kuliongezea thamani zao hilo kwa lengo la kupanua fursa za masoko.
Hata hivyo, jitihada hizi,
hazijalenga wanawake pekee, bali hata wanaume ni wamenufaika.
Miongoni mwao ni Paulo Michael
ambae alianza ufugaji nyuki zaidi ya miaka 40 iliyopita. Kwanza alianza kutumia
mizinga ya magogo ya miti kabla ya kuhamia katika matumizi ya tairi za gari
zilizotumika. Kwa Paulo, baba wa watoto kadhaa ilikuwa ni safari ndefu ya
mabadiliko katika sekta ya ufugaji nyuki.
Mizinga yake, ipo umbali wa
kilomita tatu kutoka nyumbani kwake.
Mizinga anayotumia hivi sasa
ni ile ya kisasa iliyotengenezwa kwa mtindo wa pembe nne kwa kutumia mbao
zilizopakwa rangi nyeupe na kutundikwa kwenye matawi ya miti.
Paulo anaoenekana mwenye
kufurahia kazi yake. Wateja wake wakuu ni wafanyabiashara kutoka pande
mbalimbali za nchi.
”Nimeirithisha familia yangu
ufugaji nyuki na urinaji wa asali kwa sababu tuna uhakika wa kuuza asali, ila
vikwazo ni kukosa vifaa maalumu kwa ajili ya sumu ya nyuki,” anasema Paulo,
ambae hivi sasa hamu yake kubwa, ni kukamata soko la nje, ikiwemo nchi jirani
za Afrika Mashariki.
Paulo kwa msimu mmoja wa
mavuno, anaweza kupata debe hadi 25 za asali, ambapo debe moja huwa na lita 20.
Ingawa sio kwa asilimia mia
moja, lakini Mtandao wa huo wa MVIWARUSHA umefanikiwa kuingilia kati na
kujaribu kutatua baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo wafugaji hao.
Katika hatua ambazo
zimechukuliwa ni pamoja na kutoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki, uvunaji wa
asali pamoja na mazao mengine ya nyuki kama vile masega, nta na kuendelelea.
Maria Shinini ni katibu wa
kikundi cha Emelok Enaisho anakiri ufugaji huo kuleta tija katika jamii.
Anasema, kupitia biashara ya asali, wameweza kuwapeleka watoto shule, kujenga
nyumba na hata kununua mifugo.
Moja ya mafanikio
wanayojivunia nayo ni pamoja na kuunganishwa na Shirika la Chakula Duniani- FAO
ambalo wanasema, linawasaidia kupanua wigo na kujiimarisha kibiashara.
Ushirikishwaji wa wanawake
Ushirikishwaji wa wanawake
katika harakati za kuzalisha katika jamii, umesaidia kuondokana na mfumo dume
uliokuwa umekita mizizi katika jamii hiy ya Kimaasai.
“Kwa sasa tumeondokana na
mfumo dume, na tumepata heshima kupitia ufugaji nyuki. Hivi sasa, naweza
kujikimu kimaisha na familia yangu. Awali hatukua na fursa za masoko kabisa
kwani tulipovuna asali tuliishia kuuzia ndugu na jamaa waliotuzunguka, lakini
sasa mambo yamebadilika,” alisema Shinini.
Shinini hamu yake ni kuongeza
uzalishaji wa asali, lakini hii inahitaji kuwa na mtaji mkubwa zaidi wa
kuongeza mizinga ya nyuki ya kisasa, ambapo bei ya kila mzingo, ni takriban
dola 50 za kimarekani. Shinini hivi sasa ana jumla ya mizinga 85.
Hata hivyo, safari yao ya
ufugaji haikuwa rahisi kama simulizi yake. Kina mama hawa wa Kimaasai wanakiri
kupata hasara kwa miaka kadhaa, kutokana na ufugaji na mtindo usio wa kisasa
waliokuwa wakiutumia.
Lakini hivi sasa hali
imebadilika, na heshima imejengeka.
“Sisi wanawake wa Kimaasai
tuliachwa nyuma sana, hatukuwa na uwezo wa kwenda hata sokoni, kusomesha watoto
shule na kununua mahitaji na hata kuisaidia jamii. Nililazimika kumuomba pesa
mume wangu kila kitu. Lakini sasa kwa zaidi ya miaka minne, tumefarijika mno
kwani ninaweza kujikimu,” anasema Phinini.
“Tunafurahi kwa sababu
tumeanza kuona mafanikio baada ya kupambana na wanyama wakali wa nyakati za
usiku tunapotundika mizinga," anasimulia.
Matumizi ya asali
Zao la asali hutumika kama
chakula, dawa na zao la biashara. Aidha asali hutumika kama kiambatio muhimu
kama uokaji, viwanda vya vyakula vitamu, vipodozi, vinywaji na viwanda vya
dawa.
Tanzania ni nchi ya pili
duniani kwa uzalishaji wa asali. Kuna nchi 24 duniani zinazovutiwa na asali ya
Tanzania.
Kulingana na sera ya Taifa ya
Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998 na Mpango wa Taifa wa Ufugaji Nyuki wa Mwaka 2001,
Tanzania huzalisha takriban tani 4, 860 za asali kwa mwaka. Hata hivyo, taarifa
ya mwaka 2006 ya idara ya misitu na nyuki inaonesha kuwa Tanzania husafirisha
nje ya nchi wastani wa tani 500 za asali katika nchi za Ujerumani, Uholanzi,
Uingereza, Ubelgiji na mashariki ya mbali.
Kuongeza thamani
Wajasiriamali hao wameanza
kuliongezea thamani zao la asali kwa kuchanganya na baadhi ya dawa za tiba za
asili na kuuza.
“Tumeelewa thamani ya dawa za
asili na tunachanganya na asali na kuuza. Kwa mfano, lita moja yenye dawa
tunauza mpaka shilingi elfu 30 za Kitanzania ambazo ni sawa na dola 12 za
kimarekani,” anasema.
Changamoto
Lakini mafanikio siku zote
hayakosi changamoto. Kutokana na maeneo walipo, ambayo aidha yanapakana au yapo
karibu na Hifadhi za Taifa, hivyo wanyama wakubwa kama tembo baadhi ya nyakati
huangusha matawi ya miti na kuharibu miundombinu iliyopo. Mbali na hivyo, kuna
changamoto pia ya miundombinu ya barabara kutoka vijiji waliopo wafugaji hawa
kuelekea sehemu yalipo masoko.
Wastani wa pato la asali
nchini Tanzania kwa mwaka, ni sawa na dola 320, na nta kwa mwaka huingiza kiasi
cha dola milioni 80. Mapato haya yanaweza kuongezeka kama uzalishaji utaimarishwa.



