Na Rev. Maiko Luoga – Njombe
Jamii imeaswa kulea watoto katika misingi Bora ya Imani ya Kristo na maadili ya Kitanzania ili kuandaa watu wenye hofu ya Mungu watakaolitumikia Kanisa, Jamii na Taifa kwa faida.
Wito huo ulitolewa na Askofu Essau Kahwili wa Dayosisi ya South West Tanganyika, Kanisa Anglikana Tanzania, kwenye Misa Takatifu ya kutolewa Sakramenti ya Kipaimara katika Kanisa la Mtakatifu Daniel Mtaa wa Kambarage mjini Njombe, Jumapili Tarehe 27 Septemba 2026.
“Vijana hawa wamepokea Sakramenti Takatifu ya
Kipaimara, Tunawakumbusha mzidi kuwa Imara na kuendelea kumtumikia Mungu siku zote, Wazazi tuwaandae watoto hawa kuwa Mama na Baba bora hapo baadae” Alisema Askofu Essau Kahwili.
Kasisi Canon. Andrew Matemanga wa Mtaa wa Kambarage alisema, wamefurahi kushiriki Misa na Askofu Kahwili ambae ameanza Ratiba ya kwanza ya Kipaimara katika Mtaa huo tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu.
“Viongozi na waumini wa Mtaa wa Kambarage, Tumefurahi kutembelewa na Baba Askofu pamoja na mkewe, ambae ametoa huduma ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana wetu” alisema Canon. Matemanga.
Akiwasilisha Taarifa ya maendeleo, Mwinjilisti Mariamu Mgimwa alisema, Mtaa huo unaundwa na Makanisa mawili ya Mtakatifu Danieli Kambarage na Kanisa la Sinagogi la Mtakatifu Mikaeli Soko la Mbao, ukiwa na jumla ya waumini 453 idadi hiyo ikijumuisha watoto.
Wakizungumza mara baada ya kushiriki Misa Takatifu, waumini wa Mtaa huo akiwemo Bi. Neema Mhagama, Recho Haule, Emmanuel Samson na Mathia Mkomola walieleza kuwa, Misa hiyo ilikuwa ya Shangwe kwakuwa watoto wa Mtaa huo wameingizwa katika Kundi la Kristo.
Jumla ya Wanafunzi 22 wa Mtaa wa Kambarage – Njombe, wamewekewa Mikono ya kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara na kujazwa Roho Mtakatifu, wakiahidi kumtumikia Mungu kupitia Kanisa lake Takatifu.







