Huenda umewahi kuiona ile filamu ya zamani ya Yesu inayomwonyesha Yesu akifundisha, akifanya miujiza, akisalitiwa, akisulubiwa na kufufuka. Kwa watu wengi, sura ya Yesu katika filamu hiyo imekuwa moja ya sura zinazokumbukwa zaidi katika historia ya sinema za Kikristo.
Lakini je, unamjua mtu aliyekuwa nyuma ya sura hiyo?
Anaitwa Brian Deacon, mwigizaji wa Kiingereza aliyezaliwa Oxford mwaka 1949. Kabla hajapewa nafasi ya kuigiza Yesu, alikuwa tayari mwigizaji mwenye uzoefu katika maigizo ya jukwaani na televisheni. Alipata nafasi hiyo baada ya mchakato mkubwa wa usaili na screen tests.
FILAMU ILIYOFANYA JINA LAKE LIJULIKANE DUNIANI
Filamu hiyo ilitengenezwa mwishoni mwa miaka ya 1970 chini ya uzalishaji wa John Heyman, kwa ushirikiano na Campus Crusade for Christ, ambayo leo inahusishwa na Cru na Jesus Film Project.
Filamu ililenga kusimulia maisha ya Yesu kwa kufuata kwa karibu Injili ya Luka. Kwa hiyo, sehemu kubwa ya maneno aliyosema Brian Deacon kama Yesu yalitokana moja kwa moja na Maandiko.
Kilichofanya filamu hii iwe tofauti ni kwamba hawakutengeneza kila kitu studio. Walikwenda Israel na kupiga picha katika maeneo mbalimbali yaliyohusishwa na mazingira ya matukio ya Biblia.
Upigaji picha ulianza mwishoni mwa Novemba 1978 huko Tiberias na uliendelea kwa takribani wiki 31, katika maeneo mbalimbali ya Israel, yakiwemo maeneo ya karibu na Tel Aviv na Yerusalemu. Takribani waigizaji wakuu 45 walihusika, pamoja na maelfu ya watu waliotumika kama wahusika wa ziada.
MAISHA YAKE HAYAKUWA RAHISI KWENYE SETI
Kitu ambacho tunapaswa kujua ni kwamba kuigiza kuwa Yesu hakukuwa jambo rahisi kwa Brian.
Kwa mujibu wa mahojiano yake, siku zake za kurekodi zilianza mapema sana. Alieleza kwamba mara nyingi aliitwa karibu saa 10 alfajiri, nakuanza maandalizi muda mfupi baadaye.
Alitakiwa pia kuvaa pua bandia (prosthetic nose) na kutumia nywele bandia ili mwonekano wake uendane na taswira waliyoikusudia ya Yesu wa karne ya kwanza.
Lakini kwa mujibu wa Paul Eshleman, aliyekuwa akisimamia upande wa mradi wa filamu, Brian alikuwa makini sana na nafasi hiyo kiasi kwamba alisoma tafsiri mbalimbali za Biblia kila siku ili aweze kuelewa vizuri mafundisho aliyokuwa akiyatamka mbele ya kamera.
Watu wengine waliowahi kusimulia utengenezaji wa filamu walieleza mazingira ya seti kama yenye heshima kubwa kwa kazi ya Biblia.
Lakini Brian mwenyewe alitoa picha tofauti kidogo katika mahojiano yake. Alisema kulikuwa na nyakati za mabishano kuhusu namna baadhi ya matukio yalivyopaswa kuigizwa, na kwamba mtayarishaji John Heyman alikuwa mtu mwenye msimamo mkali.
Brian mwenyewe,alikumbuka hata siku ambazo waigizaji waliokuwa wakicheza kama wanafunzi wa Yesu waligoma kwa muda wakidai malipo ya ziada. Kwa hiyo, nyuma ya ile filamu tuliyoiona ikiwa imetulia na yenye utukufu, kulikuwa na changamoto nyingi za kawaida za utengenezaji wa filamu.
Na kuna jambo la kuvutia zaidi.
Filamu ilirekodiwa katika maeneo mengi sana ili kujaribu kuifanya ionekane karibu na mazingira ya Biblia. Wakati mwingine hata walilazimika kurudia tena kupiga picha baada ya kugundua kwamba baadhi ya miti iliyoonekana kwenye picha haikuwepo katika eneo hilo wakati wa Yesu.
Hii inaonyesha kiwango cha umakini waliokuwa nao katika kutengeneza filamu hiyo.
BAADA YA KUIGIZA YESU, BRIAN ALIFANYA NINI?
Brian aliendelea na kazi yake ya uigizaji katika televisheni, filamu na jukwaani. Pia aliwahi kuonekana katika kazi mbalimbali kama A Zed & Two Noughts, The Feathered Serpent, Lillie na Emmerdale. Baadaye pia alifanya kazi ya voice acting, akitoa sauti katika michezo ya video mbalimbali.
Brian Deacon si Yesu.
Alikuwa mwigizaji aliyepewa jukumu la kumwakilisha Yesu kwenye skrini.
Katika mahojiano yake ya baadaye, Brian alieleza pia kwamba yeye mwenyewe hakujiona kama Yesu wala kama mtu anayepaswa kuabudiwa kwa sababu ya nafasi hiyo. Katika mahojiano ya mwaka 2016 alijieleza kuwa mtu mwenye mtazamo wake binafsi wa kiroho, akisema hakuwa mtu wa kulazimisha imani yake kwa wengine.
-Brian Deacon alizaliwa tarehe 13 Februari 1949, hivyo mwaka 2026 ana miaka 77.
FUNZO
Kuna somo kubwa sana hapa.
Mungu anaweza kutumia mtu katika jambo kubwa kuliko ambavyo mtu mwenyewe anavyodhani.
Brian Deacon aliingia kwenye filamu akiwa mwigizaji. Hakukuwa na mtu aliyemwita “Yesu”; aliitwa kuigiza Yesu.
Lakini maneno aliyoyatamka yalikuwa kutoka katika Injili. Na kwa miaka mingi, watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wameitazama filamu hiyo na kusikia habari za Yesu kupitia simulizi hiyo.
Hii inatukumbusha jambo
Usidharau nafasi uliyopewa kwa sababu tu inaonekana ndogo.
Huenda wewe si mhubiri maarufu. Huenda hujajenga kanisa kubwa. Huenda huna kipaza sauti mbele ya maelfu ya watu.
Lakini Mungu anaweza kutumia kile ulichopewa kuwafikia watu ambao wewe mwenyewe hutawahi kukutana nao.
Paulo alisema:
“Basi, kila mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu.”
-Wakolosai 3:23
