BANDA MEDIA BLOG

WANAFUNZI WA JITEGEMEE WATAJA MAFANIKIO YA SHULE, WAOMBA JAMII KUIMARISHA MALEZI YA WATOTO

 


NA DENIS MLOWE, IRINGA

WAHITIMU wa Darasa la Saba wa Shule ya Msingi Jitegemee iliyopo Kata ya Mivinjeni, Manispaa ya Iringa, wameeleza mafanikio mbalimbali waliyoyapata shuleni hapo huku wakitoa wito kwa wazazi na walezi kuendelea kushirikiana na walimu katika malezi na makuzi ya watoto.

Wahitimu hao walieleza hayo kupitia risala yao iliyosomwa wakati wa mahafali ya Darasa la Saba yaliyofanyika shuleni hapo, ambapo walisema wamepata elimu pamoja na maarifa mbalimbali yaliyowaandaa kukabiliana na changamoto za maisha na kuendelea na hatua nyingine ya elimu.

“Tumekua hapa zaidi ya miaka saba. Kwa elimu ya awali na msingi, tumeweza kuipata katika shule hii tukiwa shuleni hapa tumejifunza mambo mengi, ikiwemo masomo kwa vitendo na nadharia, kuishi na jamii tofauti, michezo, stadi za kazi na masuala mtambuka,” walisema wahitimu hao.

Katika risala hiyo, wahitimu walieleza pia kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa miaka mitano iliyopita.

Walieleza kuwa mwaka 2021 wanafunzi 97 walifanya mtihani na wote 97 walifaulu, sawa na asilimia 100. ,mwaka 2022, wanafunzi 97 walifanya mtihani, ambapo 96 walifaulu na mmoja hakufaulu, sawa na asilimia 98 ya ufaulu.

Walisema kuwa mwaka 2023, wanafunzi 76 walifanya mtihani, 75 walifaulu na mmoja hakufaulu, sawa na asilimia 99 wakati mwaka 2024, wanafunzi 82 walifanya mtihani, 79 walifaulu na watatu hawakufaulu, sawa na asilimia 98 huku mwaka 2025, wanafunzi 93 walifanya mtihani, ambapo 90 walifaulu na watatu hawakufaulu, sawa na asilimia 97.

Pamoja na masomo ya darasani, wahitimu hao walisema wamejifunza shughuli mbalimbali za kujitegemea, ikiwemo usafi wa mazingira na kilimo cha bustani za mboga, ambazo wameeleza zitawasaidia kuwa raia wanaowajibika katika jamii.

Akizungumza katika mahafali hayo, Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Hamid Mbata, alisema malezi ya mtoto yanapaswa kuanzia nyumbani, huku shule ikiwa sehemu ya pili ya kusaidia kuendeleza malezi hayo.

Alisema pale linapotokea tukio la ukatili au jambo linalohitaji hatua za kisheria, wazazi wanapaswa kutoa taarifa kwa viongozi na kuwa tayari kutoa ushahidi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Nitoe wito kwamba inapojitokeza jambo kama hili la ukatili wa aina yoyote, sisi wazazi na viongozi wa jamii tuwe tayari kulifikisha jambo hilo kwenye mamlaka husika ili hatua zichukuliwe. Tusiiingilie maamuzi ya viongozi wanapochukua hatua,” alisema Mbata.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Ezra Francis Msiliova, maarufu kama Eze Nace alisema anashiriki katika shughuli hiyo kwa niaba ya kampuni ya Super Sec Investment, iliyopo mkoani Iringa.

Msiliova alisema kampuni hiyo imekuwa ikishiriki katika kutoa misaada kwa jamii na kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma kwa wananchi.

Alitumia nafasi hiyo kuwashauri wazazi kuwa makini katika matumizi ya simu na teknolojia kwa watoto, akisema dunia ya sasa imeingia katika zama za teknolojia na akili mnemba (AI), hivyo watoto wanaweza kupata taarifa mbalimbali kupitia vifaa vya kidijitali.

Aliwataka wazazi kufuatilia matumizi ya simu ya watoto wao na kuhakikisha wanajua wanachotazama au kujifunza kupitia vifaa hivyo

“Wanafunzi wengi wanapomaliza masomo wanarudi nyumbani. Ulimwengu wa sasa ni wa AI, hivyo watoto wengi wanatumia simu mzazi akimpa mtoto simu anapaswa kujua kwamba anaweza kujifunza vitu vingi kupitia simu hiyo kwa hiyo ni muhimu kumfuatilia mtoto na kujua anachofanya anapotumia simu,” alisema.

Msiliova pia alisisitiza umuhimu wa wazazi kushirikiana na Serikali katika malezi ya watoto, akisema Serikali pekee haiwezi kufanikisha malezi bora bila ushiriki wa wazazi.

Aidha, alisema Super Sec Investment itaendelea kushirikiana na jamii katika miradi ya maendeleo, akieleza kuwa kampuni hiyo imechangia ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika shule hiyo.

Alitaja baadhi ya misaada hiyo kuwa ni ujenzi wa vyoo vya kisasa, uzio wa shule na uchimbaji wa kisima cha maji, huku akieleza kuwa kampuni hiyo ina mpango wa kuendelea kusaidia shule hiyo kwa kujenga jiko la kisasa na kutoa vifaa vingine vitakavyosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG