KATIBU wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dkt. Moses Matonya pamoja na watenda kazi wa Ofisi kuu ya jumuiya hiyo iliyopo jijini Dodoma wamepokea ujumbe wa wageni kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, waliofika katika ofisi hizo kwa ajili ya kujadili na kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa programu za usimamizi na utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kukabiliana na Mbadiliko ya Tabianchi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Msisitizo umewekwa juu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 ambapo serikali inaleta wito wa kuhakikisha kuwa taasisi mbalimbali, ikiwemo taasisi za dini, zinashiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa Programu hiyo, Dkt. Simeon Peter Shimbe, ameeleza umuhimu wa taasisi za dini katika kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira na kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, ambapo Ameeleza kuwa taasisi za dini zina nafasi muhimu katika kufikisha ujumbe wa uhifadhi wa mazingira kwa wananchi kupitia makanisa, pamoja na shughuli mbalimbali wanazotekeleza katika jamii.
Katika Dira ya Taifa ya 2050, uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ni miongoni mwa maeneo muhimu ya maendeleo ya Taifa.
Athari za Mabadiliko ya Tabianchi zinaweza kuathiri pia utekelezaji wa maeneo mengine ya maendeleo, hivyo hatua za pamoja zinahitajika katika kukabiliana nazo.
Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango wa miaka mitano (2025–2030), Ofisi ya Makamu wa Rais imeiomba CCT kuungana nao katika kuhamasisha na kutekeleza shughuli mbalimbali za utunzaji wa mazingira, ikiwemo upandaji wa miti kwa wingi, kushiriki katika biashara ya kaboni, kuhamasisha matumizi ya nishati safi na usafi wa mazingira ikihusisha na udhibiti wa taka, kudhibiti viumbe vamizi, pamoja na kuhifadhi ardhi oevu na vyanzo vya maji.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCT, Mch. Modest Pesha, ambaye ni Mratibu wa ACT Alliance Tanzania Forum inayotekelezwa na CCT, ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutekeza pendekezo la kuwajengea viongozi wa dini uwezo na kutambua umuhimu wa taasisi za dini katika juhudi za kutunza mazingira.
amekumbushia utekelezaji wa mapendekezo yaliyowasilishwa na CCT kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais Tar. 24/12/2024 juu ya uanzishwaji wa dawati la uratibu wa shughuli za mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi baina ya Serikali na Taasisi za Dini ili kushirikishana uzoefu, utoaji wa taarifa za utekelezaji wa malengo na mpangokazi na kutambuliwa kwa mchango wa Taasisi za Dini katika kutekeleza Dira ya Taifa, 2050.
Mchg. Modest Pesha amesema CCT imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ikihusisha hamasa ya upandaji miti kwa Makanisa 12 wanachama kupitia mipango na matukio mbalimbali ya Jumuiya ikiwa ni pamoja na taasisi, hii ni pamoja na kushiriki katika utekelezaji wa Sera ya Mazingira ya 2021-2026 pamoja na kushiriki kufanya mapition ya Sera hiyo na Mkakati wake wa utekeleza na kutokeza mapendekezo juu ya Sera husika kwa mwaka 2027-2031.
Ameongeza kuwa CCT ipo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuhamasisha jamii kuchukua hatua madhubuti za kulinda na kutunza mazingira, kakabiliana na kuendana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi na kuhakikisha kuwa rasilimali za mazingira zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, amependekeza kuwa ushirikiano huo pia uzilete taasisi zote pamoja katika kujiandaa na Mkutano wa 31 wa Mazingira Duniani utakaofanyika nchini Uturuki 2026 pamoja na unaofatia utakaofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwaka 2027.






