*Na Rev. Maiko Luoga, Anglican DSWT Habari*
Waimbaji wa Kwaya ya Mtakatifu Yohana kutoka Kanisa la Mtakatifu Yohana Nazareth Njombe, Dayosisi ya South West Tanganyika, Kanisa Anglikana Tanzania, Jumamosi Tarehe 3 Oktoba 2026, walifanya ziara ya Utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa Ruaha katika eneo la Tungamalenga mkoani Iringa.
Wakizungumza kwa niaba ya wengine, Peter Haule, Timoth Mabuga, Beatrice Kihindo na Christina Senyagwa walisema, Ziara hiyo imekuwa ya Baraka, kwakuwa wamepata nafasi ya kujifunza na kuona maisha halisi ya Wanyama pamoja na viumbe hai vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu.
“Tumepata nafasi ya kuona wanyama ambao hatujawaona tangu kuzaliwa, Tumejifunza na kutambua kazi kubwa ya uumbaji wa Mungu, Watanzania tuwe na tabia ya kutembelea hifadhi zetu ili kujifunza kwa vitendo” walisema waimbaji hao.
Ziara hiyo iliongozwa na Kasisi Canon. Christopher Tumbuka wa Mtaa wa Nazareth na Mkuu wa Eneo la Njombe Mjini alisema, pamoja na faida ya Kutalii, ziara hiyo ililenga kufanya tafakari ya kazi njema na matendo makuu ya Mungu.
“Mungu ametoa mamlaka mwanadamu kutawala Samaki wa Baharini, Ndege wa angani na Wanyama Msituni aliowaumba yeye, Hivyo Safari hii imetupa nafasi ya kuona viumbe hivyo tulivyoagizwa kuvitawala” alisema Kasisi Can. Tumbuka.
Waimbaji hao walipokelewa na kuweka kambi katika Hoteli na Nyumba ya Utalii Tungamalenga (Ruaha Tungamalenga Lodge and Campsite) inayomilikiwa na Mwekezaji, Muumini wa Kanisa Anglikana kutoka Dayosisi ya South West Tanganyika (Njombe) kisha kupata Msaada ya kuongozwa na kuzunguka Hifadhini.
Miongoni mwa wanyama na viumbe vilivyoonekana katika Hifadhi hiyo ni pamoja na Tembo, Simba, Kiboko, Mamba, Pundamilia, Twiga, Swala na wengine wengi, Kiongozi wa Utalii aliyetoa msaada wa kuongoza waimbaji alikuwa Bw. Fadhili Mtove, Kutoka Chuo cha Utalii Mkuyu Ilenga Kilichopo Tungamalenga – Iringa.








