Anglican DSWT Habari.
Kanisa Anglikana Tanzania Dayosisi ya South West Tanganyika (Njombe) , imeanzisha Idara ya Habari na Mawasiliano ili kufikisha Injili katika Mataifa yote na kuwaunganisha waumini kwa njia hiyo.
Wajumbe wa Kikao cha Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ya South West Tanganyika walioketi Tarehe 25 Septemba 2026 katika Hoteli ya Miss Eira Mjimwema Micro City Njombe, walipitisha Agenda hiyo iliyowasilishwa na Mhashamu Essau Kahwili Askofu wa Dayosisi.
Akieleza lengo la kuanzisha Idara ya Habari na Mawasiliano katika Dayosisi ya South West Tanganyika, Askofu Essau alisema, kutangaza kazi za maendeleo ya Dayosisi ngazi ya vigango, Mitaa, Dinari na Ofisi Kuu pamoja na kurahisisha mawasiliano na wadau wa Maendeleo waliopo ndani na nje ya Dayosisi.
"Kuhakikisha tunatunza kumbukumbu za kazi zetu za kihuduma na kimaendeleo, kufanya Injili yetu iwafikie wengi kwa haraka, kuibua Historia ya Dayosisi tangu 1952 hadi sasa pamoja na kuvuta watalii waje kutembelea baadhi ya maeneo yenye historia ya Kanisa na nchi yetu" Alisema Askofu Essau Kahwili.
Akitangaza Hatua hiyo kwa Wahudumu na waumini wa Dayosisi ya South West Tanganyika, Katibu wa Sinodi Kasisi Canon Asante Haule alisema, Mara baada ya kuanzisha Idara hiyo, Askofu Essau Kahwili, alimteua Shemasi Maiko Luoga kuwa Mratibu na Afisa Habari mwanzilishi.
Aidha Katibu wa Sinodi Canon Asante Haule, alieleza kuwa Idara hiyo imeanza kufanya kazi rasmi huku akialika wadau wa maendeleo, kujitokeza kuunga mkono jitihada hizi kwa kuiwezesha Idara kupata Vitendea kazi ikiwemo, Kamera za Kisasa, Kompyuta, Printa, Vinasa sauti, Simu, Maiki na Vifaa vyote vya kazi za Habari.
Idara hiyo tayari imeanzisha Mitandao ya Kijamii inayoitwa ANGLICAN DSWT HABARI inapatikana Youtube, Facebook, Instagram, TikTok, pamoja na kuanzisha Kundi maalumu la Habari kwa Njia ya Wasap linaloitwa ANGLICAN DSWT HABARI Tuma ujumbe NIUNGE kwenda 0762705839.
Toa Sadaka kuwezesha Idara hii kufanya kazi kwa upana katika Dayosisi Yetu.
