Na. Tutindaga Nkwindi, NZUGUNI
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amekagua maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Niño katika Kata ya Nzuguni, ikiwemo ujenzi wa mfereji wa kupitisha maji eneo la Kitelela ili kuzuia maji kuingia kwenye makazi ya wananchi.
Katika ziara hiyo, alikutana na Kamati ya Maafa ya Kata ya Nzuguni kwa lengo la kutathmini hatua zinazochukuliwa kujiandaa na mvua hizo na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa mfereji huo, aliwataka wataalamu wanaosimamia mradi huo kuwashirikisha wananchi wa eneo hilo, akisisitiza kuwa ushiriki wao utasaidia kubaini maeneo yenye changamoto kubwa na kupata suluhisho linalokidhi mahitaji halisi.
“Ni muhimu kuwashirikisha wananchi katika ujenzi huu kwa sababu wao ndio wanaofahamu vizuri maeneo yenye changamoto ya maji. Ushirikishwaji wao utasaidia kupata suluhisho sahihi na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua” alisema Senyamule.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri, alisema kuwa wilaya inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ujio wa mvua za elnino ikiwemo kukarabati maeneo yenye changamoto na kuboresha mifumo ya kupitisha maji pamoja na kutoa elimu wa wananchi walio kwenye maeneo hatarishi ili waweze kuhama kwenye maeneo hayo.






