
Na. Mwandishi wetu, MANYARA
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na kampuni ya Crop Bioscience iliyopo Kijiji cha Kiongozi, Kata ya Marakea, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara zimeingia makubaliano ya kushirikiana kuanzisha shamba la mfano litakalotumika kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija.
Makubaliano hayo yamefikiwa Oktoba 19, 2026 wakati Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa TFRA, Gothard Liampawe alipotembelea shamba la kampuni hiyo linaloongozwa na Mkurugenzi wake, Wilfred Mushobozi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanayofanyika Oktoba 13 kila mwaka.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Liampawe ameitaka kampuni ya Crop Bioscience kuendelea kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea katika shughuli zake za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kupata mavuno yenye tija. Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa shamba la mfano kutatoa fursa kwa wakulima kujifunza kwa vitendo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na mbinu bora za kilimo.
Kampuni ya Crop Bioscience inajishughulisha na uzalishaji wa mbegu za mazao mbalimbali, yakiwemo mahindi, choroko, maharage na migomba. Ushirikiano huo unatarajiwa kuwawezesha wakulima kupata elimu itakayowasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.




